Maneno ya Okwi kwa waliokata tamaa ya kuwatoa Al Masry

  0

  Maneno ya Okwi kwa waliokata tamaa ya kuwatoa Al Masry

  ***Asema Al Masry wanafungika, wataenda kuwashangaza kwao…
  MSHAMBULIAJI tegemeo wa Simba, Emmanuel Okwi, amesema kuwa hana hofu yoyote na mchezo wa ugenini wa marudiano wa mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry na kuongeza kuwa Waarabu hao wanafungika.

  Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa itawafuata Al Masry katika mechi ya marudiano utakaofanyika Machi 17 mwaka huu katika mji wa Port Said.
  Akizungumza nasi ,Okwi, alisema kuwa watapambana kuhakikisha wanashinda na mechi hiyo ya marudiano haitakuwa ngumu kama ya juzi kwa sababu tayari wameshawafahamu wapinzani wao.

  Okwi alisema kuwa anaamini benchi la ufundi litayafanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mechi ya juzi na hatimaye kuwadhibiti Al Masry na kusonga mbele katika michuano hiyo inayoandaliwa kila mwaka na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

  “Mechi ilikuwa ngumu lakini tuliongeza bidii na kufanikiwa kusawazisha, kikubwa hatukupoteza mechi na tunao uwezo wa kuwafunga huko kwao kwa sababu hatutaenda kuzuia,” alisema mshambuliaji huyo wa timu ya Taifa ya Uganda.

  Naye Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Masoud Djuma, amesema kuwa wanamshukuru Mungu hawajafungwa katika mechi ya kwanza na dunia ya sasa timu zinaweza kushinda ugenini na kusonga mbele.

  “Vijana walipambana kwa nguvu kuhakikisha wanapata mabao, mpira ulikuwa mgumu katika kipindi cha kwanza lakini kipindi cha pili kilikuwa chetu ila umeme na mvua vilituharibia, yote ni mipango ya Mungu lakini tumelinda heshima ya kutofungwa nyumbani,” alisema kocha huyo.
  Simba ambayo inaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara itahitaji ushindi wa aina yoyote ili waweze kusonga mbele katika mashindano hayo lakini ikitarajia kuanza mazoezi leo kwa ajili ya mechi za ligi ya hapa .

  source nipashe

  NO COMMENTS

  LEAVE A REPLY